Om Tungo Zetu
Wataalamu wa lugha na fasihi na mila za watu mbalimbali wametuzindua juu ya utajiri wa fasihi ya Waswahili. Katika fasihi hiyo, tungo za Kiswahili ndilo jambo lililojitokeza mbele kwa mwanga wenye kunawiri sana. Profesa Ibrahim Noor Shariff amefanya utafiti mkubwa kabla ya kukiandika kitabu hiki. Natija yake ni kuwa yaliyoelezwa humu yametufunulia mengi yaliyokuwa dafina. Tokea 1988 kilipochapishwa kitabu hiki kwa mara ya kwanza kimekuwa ni kitabu cha kukirejelea kwani kinaeleza yale ambayo watungaji wa tungo za Kiswahili, wataalamu, waalimu na wanafunzi wanaotaka kuelewa khabari za tungo huwa wanakirejelea mara kwa mara ili kupata jawabu za masuala yao.
Kitabu hiki kimepangwa vizuri sana kwani kila maudhui yameandikwa chini ya kichwa cha khabari kinachoelezea maudhui yanayofuata. Hali kadhalika, kitabu kina mifano ya tungo za kupigiwa mifano. Yoyote anayetaka kuzungumza khabari za tungo za Waswahili hataweza tena kujadili mengi ya maana iwapo atajinyima fursa ya kusoma yaliyoandikwa katika kitabu hiki cha Tungo Zetu.
Vis mer